Sunday, October 7, 2012

Mwanadamu akipanga



Kwa jina ninaanzia, la Mola muabudiwa,
Mshirika asokuwa, hakuzawa, hakuzaa,
Shiriki aichukia, na kaionya dunia,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Kila unalolilenga, yafaa kukusudia,
Akatunuku kwa kinga, upate kufanikiwa,
Ukijifanza kuringa, hatiani hukutia,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Jema ukikusudia, haachi kuangalia,
Kwa kiasi likakua, hadi lipate komaa,
Na thawabu unapewa, nyingine usizojua,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Baya ukikusudia, unaweza kuachiwa,
Ila kamba inakuwa, mwenyewe kujinyongea,
Itihari umepewa, kati yake kcuhagua,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Milango huifungua, kwa dua wanaojua,
Hadi ndani kuingia, tusikokufikiria,
Mutumaina wakawa, wenye enzi majaliwa,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Kidogo nilichopewa, kikubwa kimeniwia,
Nahofu kikizidia, shetani kunisifia,
Hilo dhambi litakuwa, twaha ikanikimbia,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Nje ninachungulia, vilango vya kupitia,
Kulikofungwa si njia, kati nisijeishia,
Mwanga unaponijia, papo hapo 'taingia,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Ahadi naililia, ninangojea  kupewa,
Mola nakutegemea, kuiachia ridhaa,
Hapana wa kunifaa, kwako ninaelekea,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

Inahuu yakiduna, wa akiduu kaida,
Katamka maulana, aso tadi wala inda,
Nashukuru Subuhana, mja unayenilinda,
Mwanadamu akipanga,  mola naye anapanga!

No comments: