Sunday, October 7, 2012

Nchi husambaratika



Fedha ikipotea, kwa uovu kutetea:
Mamia yakatumiwa, kwenye mambo yasiyokuwa,
Huku wafa wengi njaa, walia kimya kimya:
Nchi husambaratika!

Amani  ikipotea, kwa mabaya kuyazua:
Nchi mkaichukia, na kumaliza raia,
Kiumbe hapatakuwa, nchini kumuangalia,
Nchi husambaratika!

Umoja ukipiotea, kwa watu kuwanunua:
Kisha ukawatumia, kama vile ni bidhaa,
Upate kufanikiwa, huku yao yanavia,
Nchi husambaratika!

Hekima ikipotea, na ujinga kuuoa:
Maamuzi kuamua, nchi yanayoipasua,
Nyufa zikatokezea, kila mahala kujaa,
Nchi husambaratika!

Busara ikidumaa, ikatawala mizaha:
Huutumbua usaha, mauti kuwa nazaa,
Na kila anayejua, njia hiyo huambaa,
Nchi husambaratika!

Ujamaa kujifia, na ubepari kuingia:
Zikatawala tamaa, na  ukubwa kujitia,
Maualana huamua, aibu akawatia,
Nchi husambaratika!

Usawa ukipotea,  tofauti kubwa kuwa:
Tabaka kufurahia, na wengine kuringia,
Vya msingi vilokuwa, watu hawana wakawa,
Nchi husambaratika!

Haki ikinunuliwa, na wengine kuuziwa:
Mnyonge akaumia, mwenye nguvu kufurahia,
Juu vipofu wakawa, kwa kuvaa miwani ya jua,
Nchi husambaratika!

No comments: