Sunday, October 7, 2012

Shikilieni huko juu

Ghorofa mliyojenga, mmejenga akilini,
Kwa yetu mkatukaanga, kwa mafuta ya mwilini,
Njaa yenuu mkaganga, na matumbo kuyawini,
Shikilieni huko juu, sisi chini twabomoa!

Ya chini mmeyasonga, hali yetu taabani,
Hali nyie mnajenga, twazidi kurudi chini,
Halafu mnatukonga, bado mwachoma ubani,
Shikilieni huko juu, sisi chini twabomoa!

Mwatugeuza mizinga, kufyatuliwa vitani,
Nafsi zetu  kuchonga, ukweli tusibaini,
La kweli hamtalonga, mchawi kmbaini,
Shikilieni huko juu, sisi chini twabomoa!

Mgongoni mmepanga, ili muwe kivulini,
Na sasa tunajipanga, kuwaondoa mwilini,
Na pasipo kuwaenga, tukawatupa juani,
Shikilieni huko juu, sisi chini twabomoa!

Msingi tunaujenga, uwe mpya mwakani,
Kazi tuliiboronga, jamvi na tulisukeni,
Kuchimbua, kuchabanga, vibarua ganganeni,
Shikilieni huko juu, sisi chini twabomoa!

No comments: