Tuesday, September 4, 2012

DHULUMA YA UUAJI



MAMBO yanapoanzia, kila mtu bize huwa,
Hakuna wa kufikiria, na sababu kuijua,
Huhangaika na dunia, hadi yakikuzungua,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Huyo aliyeuawa, si wa kwetu alikuwa,
Msiba tumesikia, wala hatukumjua,
Nani angemlilia, licha ya kumchangia,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Kawaida tulijua, na kukubali kuambiwa,
Nchi inaendelea, na usalama yajaa,
Kikombe kimetulia, kumbe chini chavujia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Mwingine akafatia, hakutoka wetu mkoa,
Hayo tulipyajua, wala hatukujistua,
Huzuni ikaambaa, nani kumsikitikia?
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Machozi yakasinzia, na macho yakalemaa,
Si wa wetu mkoa, nini kujihangaikia,
Kaida tukapanua, kiada lililokuwa,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Juzi aliyeuawa, si wa yetu wilaya,
Mbali sana katokea, kwenye zege na maziwa,
Ikawa kujisemea, bwana katoa, katwaa!
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Innali lillahi pia, wa inna illahi pia,
Rajiuni tukatia, imani kuifatia,
Kwani hatukutambua, wala asili kujua,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Kadari tukaamua, mbele ametangulia,
Nyuma tunafuatia, bila ya kuhujumiwa,
Shetani katuhadaa, yote sawa kudhania,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Daktari kaibiwa, kama vile ni bidhaa,
Msituni katupiwa, wakidhani kajifia,
Fisi atamfagia, wasafi wakabakia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Walimu wanahofia, kitanzi chaning'inia,
Vitisho wavipokea, bila watu kuwajua,
Watumwa au watumiwa, hilo hawajalijua,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Mwislamu kumkwaa, chini kaangukia,
Watu tukaangalia, moyoni twajisemea,
Mkorofi amekua, haki yake kupigania!
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Njiani kumuachia, sisi tukafikiria,
Nguvu ameshaishiwa, kaanguka kwa njaa,
Pale hatukumnyanyua, sembuse kumchangia?
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Alipopaangukia, wala hatukuanglaia,
Wenyewe tukaamua, akili hakutumia,
Kawaida tukavaa, desturi kwendelea,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Mwingine akauawa, dini yetu asokuwa,
Sisi tukajikalia, ya kwetu kuangalia,
Kama vile tunajua, sisi hayatatokea,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Mwingine akauawa, kabila letu hakuwa,
Mmakonde kazaliwa, chamaki mchanga kaua,
Mzaramo kamkimbia, kamuacha auawa,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Kisha akafuatia, kibaka tunayemjua,
Siku haikuishia, mwana wetu kazuliwa,
Pale alipofumaniwa, wizi akasingiziwa,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Tairi wakamtia, na moto kumuashia,
Mwana akateketea, huku tunamuangalia,
Mwanamke katujia, si mwizi atulilia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Sadaka ilishakuwa, hakuna cha kubakia,
Kafara ametolewa, kwa sheria za kuzua,
Na hii ndiyo tabia, wakuu wafurahia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Hadi yanapotokea, kwenye zetu familia,
Ndipo macho hufungua, ukweli kujipenyea,
Shetani katwiingilia, ovyoovyo anaua,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Islamu kuhiniwa, sawa tukakubalia,
Bila ya kujitambua, kibao kugeuziwa,
Mwenzio akinyolewa, maji tumeyakataa,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Usafi tukajitia, mkorofi amekua,
Na nyimbo kuwatungia, zaidi kushindilia,
Huku tunafurahia, waumini tutazoa,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Tusipozidi wafaa, budi kutugeukia,
Na chote tulichopewa, huenda wakatukua,
Utupu kutuachia, tubaki tunayajutia,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Kifua ukimkingia, bei hukupandishia,
Walimu hawatakuwa, hilo wakakubalia,
Huanza kukuhesabia, kama huna wakuua,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Kibao hukugeuzia, kazi uliyewapatia,
Ndivyo ilivyo dunia, na huko mnaelekea,
Laiti mkijitambua, maafa mtazuia,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Fikra mkipakua, salama kujidhania,
Walokole mlokuwa, kuwa hamtajaribiwa,
Huishia kuyajutia, wakati ukiwadia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Katika hii dunia, wajaa watu wabaya,
Nchi wakiichukua, hakuna cha kuambulia,
Hao ukisadia, mtegoni waingia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Wauaji hutumiwa, kazi zao kuwafaa,
Shetani awatumia, kwa uhai kuutoa,
Wao wakifikiria, ndio eti wajikwamua,
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Katoliki wadhania, ufalme wautwaa,
Kibao kugeuziwa, muda hautachukua,
Haya mtajayajuti, laiti mngelijua,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Sote panapotufaa, ni adili kulilia,
Haki tukaisimamia, na usawa kuridhia,
Vingine haitakuwa, wenyewe tutaumia,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Ni mafundi wa kugawa, vitani mkaingia,
Wenyewe kujiumbua, pasiwe cha kubakia,
Kisha hufurahia, usukani kuutwaa,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Shetani akiingia, nani wa kumridhia,
Kati yetu huchagua, Islamu na wasokuwa?
Au wote huvamiwa, imani kutuondoa?
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Sauti mnatakiwa, viongozi kuitoa,
Dini mnaosimamia, la kwenu tukasikia,
Haya mkivumilia, pabaya twaelekea,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!

Nusura kwetu kwanzia, pengine haitatokea,
Ni bure tutajihadaa, watu hawa wanshalewa,
Vigumu kufikiria, iwe ndio kutambua ?
Muuaji akianza, hujui anayefata!

Hofu zinawachochea, za uongo zikitiwa,
Adui wakamdhania, hata yule asokuwa,
Risasi waziachia, kila mahala kupaa,
Kazi yake akianza, muuaji hachagui!


No comments: