Tuesday, September 4, 2012

TAIFA WENYE KUUA







UMUNGU akijitia, kutaka yote amua,

Hoja akazikataa, za kweli zilizokuwa,

Na uongo kutumia, umma akauhadaa,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Hawezi kuwa raia, dola hii hakupewa,

Huyo anayeshilkilia, atakiwa kulijua,

Mamboye yanavyokuwa, ndivyo nchi nayo huwa,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Dola akiitumia, wengine kuwachukia,

Kisha akapendelea, wa kwake waliokuwa,

Nchi huwa anaua, huku ashangiliwa,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Akizidisha tamaa, na ukubwa kuutwaa,

Watu kutowaachia, uhuru wa kupumua,

Akajifanza wa kujua, hata asiyoyajua,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Watu wakimtumia, walo nyuma ya pazia,

Yao akayasikia, bila kiini kujua,

Wala wana ipi nia, mbele iliyotangulia,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Yakishindwa kutimia, aliyoyafikiria,

Ubaya akawatia, wabaya wasiokuwa,

Kisha kuwashambulia, kwa maneno na silaha,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Hawezi kuwa raia, hii si yake himaya,

Hazina hawajapewa, kwa lolote kuitumia,

Wakiamua mabaya, basi maovu huzua,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Mpinga demokrasia, kisirisiri akawa,

Huku anabwabwajia, mema anatutakia,

Ndumilakuwili huwa, vyema hivyo kumjua,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Watu mwenye kuwagawa, visenti kuwapatia,

Wao wakishajaliwa, wengine watafatia,

Udokozi wakazua, nchi kujitafunia,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Hakuna kinachobakia, uongo watauzua,

Huyu tumemmegea, hata na ndugu zako pia,

Na kinachofuataia, wengine kuwa wabaya,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Hekima akiivua, ujinga ukawa kisiwa,

Busara akifukia, utoto kuogelea,

Roho huwa zajifia, aidha mioyo pia,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Na wasiojitambua, hili watashingilia,

Kaburini huingia, huku wanachekelea,

Mumiani kumwamkua, machinjoni waingia,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!



Ndio sana yatakiwa, katiba kutuamulia,

Dhima kumpunguzia, asitupeleke pabaya,

Mungu tukimdhania, Mola hatolifurahia,

Nchi anayeiua, ni viongozi wa nchi!

No comments: