Tuesday, September 4, 2012

Akuvutaye kwa udi

KWA udi akuvutaye, mvujewe hukutoa,

Hapo ndipo yaishie, kwake yako yalokuwa,

Kiwewe asikutiye, ukweli ukamjua,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Wakati akutakaye, marashi atayatia,

Pumzi asiachie, kila kona kunukia,

Nasibu aingojee, wewe kumkumbatia,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Uoza ni afichaye, yake kutokuyajua,

Vingine usimfikirie, mkweli ukadhania,

Kumbe akuhadaa weye, yake akafanikiwa,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Ni mtu ajipambae, kwa sifa asiyokuwa,

Cheo juu ajipae, muhimu ukadhania,

Ili yoe yake yawe, bila ya wewe kujua,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Ni msafi ajifanyae, kama vile hana doa,

Ili kwa wamjuaye, waijua yake tabia,

Kabisa si wamtakaye, mbali naye wanakaa,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Uzuri kama kinyaye, hakika huutumia,

Ili wasimtambue, si kitu aliyekuwa,

Jamili yake ni koe, chambo chake kuvulia,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Kinda huwa avizie, kitu wasiotambua,

Mwepesi adanganyae, sura kutokufichua,

Wakaingia kiwewe, kwa bashasha kuwatia,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Si mtu afunuaye, ukweli huuchimbia,

Kamwe juu asitoe, mkaa akapalia,

Si nuru atakaye, nuru huwa akataa,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

Mishtuko jiandae, ikiwa wamkurubia,

Na silaha uitwae, joka akigeukia,

Kisogo usimwachie, nondo atakuangushia,

Akuvutaye kwa udi, hukufukuza kwa mvuje!

No comments: