Tuesday, September 4, 2012

MTOTO AKIONGOZA





Yenyewe yajiendea, hakuna asiyejua,

Mwana akizawadiwa, maajabu atazua,

Njaa asiyeijua, na watu kupendelea,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Kama kweli kalelewa, wananchi hatotwibia,

Chetu ataangalia, na kisha kukipigania,

Nafasi ikitokea, azidi kutuongezea,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Umeme hatotuhadaa, kwa trilioni kufua,

Ujanja atatumia, njia zetu kuzijua,

Umeme tukakamua, kama vile ni maziwa,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Fedha hatotuibia, Uswizi kujifichia,

Tamaa haitwamtaa, ukubwa kuulilia,

Utoto atatezea, ya kwetu yakawadia,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Rushwa ataikataa, maana hana mazoea,

Takukuru kujifia, haki bado ikakua,

Akaondoa udhia, nchi ikarehemewa,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Hatutakuwa na njaa, kilimo sio sanaa,

Masoko kuulizia, ndio mbegu akatia,

Mlaji akanunua, na sio kununuliwa,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Michezo hatutafulia, uwanja kauchagua,

Kucheza ni mazoea, wala sio kujitia,

Jinsi anvyoshangilia, medali tutazivua,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Amani atatambua, ulinzi hajaupewa,

Mungu katusaidia, kuitunza twatakiwa,

Hawezi kuichezea, kwa ukubwa kujifaa,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Umoja ataujua, hustawi pasipo njaa,

Chakula atawania, bei zipate pungua,

Kama ulaya ikawa, chini ya kumi asilimia,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Kama ulaya ikawa, chini ya kumi asilimia,

Kipato kinachoingia, kwa chakula kutumia,

Kingine kikabakia, tutaacha kuendelea?

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Mola tunamlilia, utoto wa kutufaa,

Si ukubwa wa nazaa, watu waliojichokea,

Nakisi yaendelea, na nafuu inapaa,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!



Kisha wanajipikia, takwimu za kutungua,

Uongo zilizojaa, ukweli zinaoua,

Eti tunaendelea, huku twazidi fulia,

Ukimkabidhi mtoto, nchi hii aongoza!

No comments: