Sunday, November 6, 2011

Mkoloni sio rangi

Fikra za kale kando, mfumo wa vyama vingi,
Waliozoea uhondo, wanayo maswali mengi,
Umma kukosa vitendo, uongozi hauringi,
Mkoloni sio rangi, ni fikra na matendo.

Watu wachoka uvundo, kasumba na hizo bangi,
Kupenda bila upendo, wakataa kina mangi,
Waita huo utondo, wasusa nayo shilingi,
Mkoloni sio rangi, ni fikra na matendo.

Wenye akili mgando, wavigwaya vyama vingi,
Kumbe ni kusaza kondo,machungu kuzua mengi,
Halihitaji dondoo, kokeni sio mirungi,
Mkoloni sio rangi, ni fikra na matendo.

Yuwapi mwanakondoo, afaaye watu wengi,
Tumebakiza mapindo, japo wavaa ushungi,
Ubinafsi kuwa kando, kwao halina msingi,
Mkoloni sio rangi, ni fikra na matendo.

Wauaji bila nondo, na kuiba hawavungi,
Nchi haina mkondo, yanavuja maji mengi,
Na mengine kwenda kando, wala wanga hawawangi,
Mkoloni sio rangi, ni fikra na matendo.

UKoloni ni uhondo, kuufaidi kwa wingi,
Masazo kuweka kando, na vipande vya vichungi,
Ukawa wao msondo, maskini walo wengi,
Mkoloni sio rangi, ni fikra na matendo.

Wenye vichache vitendo, pasi manufaa kwa wengi,
Moyoni wenye mafundo, kujilimbikizia vingi,
Wengine kuweka kando,wakose hata msingi,
Ukoloni sio rangi, ni fikra na vittendo.

Mweusi kama Mngido, kabla huwa haringi,
Ukimpatia uhondo, humshinda hata mengi,
Akajiona wa mwendo, wa dola sio shilingi,
Ukoloni sio rangi, ni fikra na vittendo.

Si watu wa vitendo, la wengine hawajengi,
Kujisunda ndio mwendo, sio leo mara nyingi,
Na kukusukuma kando, ndio wao mlangilangi,
Ukoloni sio rangi, ni fikra na vittendo.

Huo ni wao mtindo, tena ni wa siku nyingi,
Kubadilika kibindo, hili kwao hawapangi,
Hujiona wenye windo, wengine mbuzi wachungi,
Ukoloni sio rangi, ni fikra na vittendo.

No comments: