Tuesday, September 7, 2010

APARTHEID TANZANIA

1.
Wanavijiji walia, wao hawana thamani,
Nchi hii inakua wao wako mkiani,
Na tunayojivunia, wenzetu hawayaoni,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
2.
Kama haujatembea, nenda sasa vijijini,
Kila kitu chazubaa,ni kinyume cha mjini,
Huduma zimelemaa,na usafiri msibani,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
3.
Nchi kama haijajua, walioko vijijini,
Hesabu ukikokotoa, ni asilimia tisini,
Na kidogo wazidia,ninasema yumkini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
4.
Barabara zaduwaa, washindwa kuja sokoni,
Kama isingelikuwa, kwa simu za mkononi,
Mawasiliano pia, yangekuwa mashakani,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
5.
Nyumba zao zatitia, udongo uso thamani,
Japo tungeliamua, pawe ujenzi makini,
Hili lingelitokea,kunusuru masikini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
6.
Bado haijatokea, lakini mwetu moyoni,
Kulola twaendelea, maamuzi hatuoni,
Miaka inajongea,wazidi umaskini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
7.
Miradi tungevumbua, kama vile kampuni,
Watu macho kufungua,hisa waweke kapuni,
Yao kushughulikia,huku wapata mapeni,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
8.
Maji na umeme pia, vingeliingia ndani,
Wengine tungehamia , hukohuko vijijini,
Mjini tusingechagua, nani ataka foleni?
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
9.
Apartheid yaua, maendeleo vijijini,
Wizara zingehamia,pande zote mikoani,
Neema ingesambaa,upungue umaskini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
10.
Dar sasa imekuwa, ndio kwetu duniani,
Kila kitu kinajaa,vya ovyo na vya thamani,
Mitaa sasa kinyaa,na kesho haina yakini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
11.
Bajeti tunayoandaa, kwa sasa ya kizamani,
Rasimu tungelitoa,washauri vijijini,
Mengi tungeliamua,uchumi uwe makini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.
12.
Hapa mwisho naamua, faida tena sioni,
Nimeshapurukuchua, tongotongo za machoni,
Wenyewe nawaachia, mwanga mje kuubaini,
Apathedi Tanzania, mjini na vijijini.

No comments: