Tuesday, September 14, 2010

Redio zetu ngumbaru

Chururu sio ndururu, jambo ni kuendeleza,
Hapo tulipo kufuru, redio zatupumbaza,
Hazitupi kuu duru, za hali zetu kukweza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Vituo vyetu ngumbaru, elimu vinaikwaza,
Nasema staghafiru, takataka waeneza,
Akili zawa kiguru, hazina zinazoweza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Sijaona la kushukuru, labda wachache waweza,
Clouds wanadhukuru, na Times wanajikaza,
Wengine waanza zuru, spidi budi kuongeza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Watangazaji ngumbaru, silabi wanateleza,
Hawafai wakufuru, na thamani wapoteza,
Chuo waende kuzuru, yapasayo kujifunza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Vyombo vinataka nuru, visheni yenye kuweza,
Ili vifanye kadiru, na watu kuwaongoza,
Wasiwe kwenye tanuru, la fikra zenye giza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Na beleshi na sururu, chimbeni yenye kukuza,
Hatimaaye tufuturu, vitamu vya kutukuza,
Wazee na barubaru, waweze kujiendeleza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Lazima muwe vifaru, wa ajenda kutangaza,
na kisha kwenye kukuru, kakara za kuyahimiza,
Hata yakiwa msururu,nchi nzima kuyaeneza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Redio ni chombo cha nuru, hakijawa ni cha giza,
Yabidi kujikusuru, kazi yake kuifanza,
Changamoto si kuzuru, bali ni kutekeleza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Ni tausi si kunguru, sifa yake naijuza,
Ni mtori si kiburu, hili ninawachagiza,
Ni changu wala si nguru, yafaa kujitangaza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

Tuondokane na ngumbaru, lazima kujiendeleza,
Msiifanye kufuru, kudhani sasa mwaweza,
Safari bado kuzuru, vingine mwajilemaza,
Radio zetu ngumbaru, nguvu yake kupumbaza.

No comments: