Tuesday, September 14, 2010

Mja kalipenda tumbo

Mja kafanya vijambo, kaacha wake umimi,
Kazishinda zake tambo,na sasa huwa hasemi,
Kakoma pia vikumbo,yapata miaka kumi,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Nimemuoana kwa GUmbo, pasipo ya kutaraji,
Kashabihiana na tembo,mnyama sio la maji,
Kidogo niende kombo,kudhani mnenguaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Ingelimdanda nembo,hadi kuja wasemaji,
Na baada ya zao jambo,kutaja wahusikaji,
Akili kama mgambo, hakuna ufikiriaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Mhariri kanywa tembo,kasahau upangaji,
Marejeo kwake chombo,wazidi utumiaji,
Na wasanifu ni chambo,hawadhibiti ujaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Tumbo keshapendwa tumbo,kila saa wamhitaji,
Usimseme kwa fumbo,ana wake wasakaji,
Ila hajawa mrembo,kulewesha hana beji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Si wa Komba si wa Bambo,wote hawana msemaji,
Tumbo hajashikwa tumbo,asingediriki ulaji,
Hajui kwenda umwambo, alale kama mfungaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Na hakai kwa kitambo, tabia mngurumaji,
Huyafanya majigambo, utadhani mtangazaji,
Na mara huimba nyimbo, japo sauti haiji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Hajajua hili tambo, linataka upangaji,
Ngwee tatu weka mambo,Ziwe na ukamilikaji,
Ya shibe iwe ng'ambo,mbili fanya usakaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Hauhitaji kimombo, kujua maji wahitaji,
Na hewa iso na shombo, fanya wake uwekaji,
Utaliafua tumbo, liache ulalamikaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Sikuzidisha urembo, labda mchapishaji,
Na mhariri mgambo,kaufanya ufujaji,
Sina mahaba na tumbo,kiasi mchokonoaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

Na Korie haiwi Kimbo, si mmoja uchakachaji,
Na mtu huwa isembo, wasemavyo wazaaji,
Halijali lake umbo,likikosa usagaji,
Mja kalipenda tumbo, litakacho halinyimi.

No comments: