Wednesday, September 15, 2010

Ujauzito wa moyo

Usiombe kuwa nao, ujazito wa moyo,
Omba uepushwe huo, usife kwa jakamoyo,
Ni pepo wa vipepeo, viumbe wapepeao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa hila, wa mengi tuyatakayo,
Fikira na masuala, wakubwa wapuuzayo,
Ni jumla kwenye sala, na sadaka watoayo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Hutesa ukiwa macho, fikra kuwa kaziyo,
Kwa dhahiri na kificho, huwaza yale yasiyo,
Husaga kama pikicho, ya chini juu yawayo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Mimba ya maendeleo, mashujaa wabebayo,
Haina katu uzio, kutesa nyoofu nyoyo,
Mema wawatakiao, wenzao bila uchoyo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Si uongo ninenayo, ni wengi wawajuayo,
Roho mbaya wakataao, na washindao choyo,
Mitihani wavukao, na ng'ambo wasogeao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ni chini warudiao, wakapafanya makao,
Wanyonge wanyanyuao, ili kuja juu nao,
Na ukubwa wacheleao, usio katu mafao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Si bendera wapepeao, wananchi wawavungao,
Ni jasiri wa matao, na uchumi wajengao,
Ni amiri wa mgao, haki waisambazao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Si kwa sifa watembeao, ila mbegu waletao,
Si mashabiki wa bao, bali waletao ngao,
Wanyonge lao kimbilio, ndio kubwa tegemeo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Watu wa matarajio, ndoto watafsirio,
Na mwanga wauletao, si gizani wakaao,
Pia na wazungukao, mwangani wawachukuao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa moyo, ndoto zake za kioo,
Muhali urejeshao, maono ya matokeo,
Na wa nje wajuao, ni wachache wapatao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa moyo, ni simanzi ubebao,
Kwa yote uonayo, na hayo usikiayo,
Na yake matamanio, kuwa nao kifananio,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa moyo, washinda ule wa tumbo,
Ni mengi myasemayo, siyajali majigambo,
Ni walevi mlewao, kila aina ya tembo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Machache myajuayo, ila ndio mjionao,
Waibaji vidakao, hupora vyetu na vyao,
Ukubwa wautakao, japo sio wajengao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

No comments: