Sunday, September 19, 2010

Wachawi saidieni

Sifa zenu naamini, zimeenea mjini,
Kadhalika vijijini, pia kote duniani,
Kwa kweli twawaamini, ila bado kuwathamini,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Mtunzi nimebaini, mna mengi kwa yakini,
Mwaweza fanya nchini,uchumi usiwe duni,
Mkaongeza thamani,dunia kututhamini,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Tunataka televisheni, zenye bei afueni,
Mwazitengeza nyumbani, hamuuzi madukani,
Tunachotaka mwakani, hizo ziwe mitaani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Mwazungumza hewani, ila simu hatuoni,
Nalo hili twaamini, ni biashara auni,
Zije simu za mkononi, tuwe nasi washindani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Finland na Marekani, kwa Nokia ni makini,
Motorola nayo ndani,Ya kwetu iwe akilini,
Tuuite jina gani,pengine la Majinuni,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Mashine kaziundeni, tupeleke viwandani,
Msukule watumieni,hata nishati wabuni,
Ili mradi mwakani,nchi iwe namba wani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Na ungo kageuzeni, tupate ndege angani,
Eitisii ifufueni,iende hadi Japani,
Na mizigo tubebeni,tuiuze kwa jirani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Elimu yenu ya ndani,mwaisaka ugenini,
Kadhalika mashambani, pamwen namo nyikani,
Vilevile vichakani, yote mnayathamini,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Majongoo geuzeni, wawe za sasa treni,
Dizeli iachieni, umeme tutumieni,
Uchina shirikianeni,mwokoe zetu laini,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Maji huko maziwani, uchawi utumieni,
Yapande hadi nyikani, tunyweshe mashambani,
Tutumie na mjini,maana hayaonekani,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Mwingie na baharini, madini yatafuteni,
Pia mafuta sakeni, nchi ipate ihwani,
Haya sifanyi utani,wallahi ninawaamini,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Mmeshinda mitihani, wajao uongozini,
Mliita mashetani, mizimu pia majini,
Hiana hawakuwafanyieni, wakawa madarakani,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Hakika nawaamini, nchi yawategemeeni,
Bila ya nyie yakini, tutakuwa mashakani,
Kuendelea yumkini, pasiwe matumaini,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Kama wanawaamini, viongozi duniani,
Basi ni nyie makini, na si wao jamani,
Ustawi uleteni, daima tuwasifuni,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

No comments: