Wednesday, September 15, 2010

Nyumba kwa kila kaya

Ndoto zingine uchizi, ota kinachowezekana,
Sitaki kupiga mluzi, waelewa waungwana,
Zimepita fumanizi, na ahadi za laana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Msusi sio kinyozi, hili si la kubishana,
Na viazi sio ndizi, ijapo vinalingana,
Mmoja juu hawezi, na mwingine chini huchina,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Baradhuli na bazazi, hawajui la maana,
Saa zote kinywa wazi,japo mambo si bayana,
Kwao fikra si kazi, kwa hewala ni watwana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Nchi haipandi ngazi, hadi makazi kusana,
Wananchi wawe wakazi, si wakimbizi aina,
Hayahitaji mjuzi, haya yako wazi sana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Haugharimu ujenzi, twamiliki zote zana,
Vifaa havina kazi, rahisi kupatikana,
Fundi wako kwa majozi, kila fani waoana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Nchi yetu pandikizi, viotani twabanana,
Magenge yetu makazi, na hamna muamana,
Roho mbaya twatarizi, choyo na nyingi hiana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Nchi yetu bado wazi, mbona tunaumbuana,
Wanazuka majambazi, tuliowapa dhamana,
Wauza viwanja wazi, kisa twataka banana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Vyauzwa viwanja wazi, huku twavumiliana,
Watoto wakosa malezi, bado tunachekeana,
Wehu twawapa hifadhi, nchi yazidi gongana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Twasemwa ni wapuuzi, wala akili hatuna,
Mambo yetu ya kishenzi, wala sio waungwana,
Hili wala hatuwazi, ni kama sawa twaona,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Ufukkara sikuhizi, ni sifa yenye laana,
Hukuhama wanunuzi, mbaki kuangaliana,
Nao pia watembezi, wakawa hawaji tena,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Umasikini kitanzi, wenyewe tunanyongana,
Nchi yataka wajenzi, sio vitu vya Wachina,
Nchi yataka makuzi, na sio kuchomoana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

No comments: