Wednesday, September 15, 2010

Kwanini ni masikini

Sisi sio masikini, ila uongozi duni,
Fikra za walakini, ndizo tunazothamini,
Na twawaona wageni, eti ndio wenye thamani,
Wenyewe hatujithamini, vipi tuwe na thamani ?
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Hawamjui Auni, na fikra Muhayamini,
Nadra kwa afueni, kwenda kwa watu wahuni,
Unyama na uhayawani, sio ya kwetu amini,
Uungwana duniani, huanzia kwako nchini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Mbele sana hatuoni, njaa yetu twabaini,
Kaumu haina ihsani,na mifumo walakini,
Dira yetu ni maoni,na wala sio ramani,
Tatizo hatulibaini,vipi uishe umaskini ?
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Nafsi zetu lawamani,si watu wenye imani,
Vitabu hatuvioni,Kuvisoma si yamkini,
Vitakatifu shakani,vya kawaida kapuni,
Wamezuka wajuwani,kila kitu wabaini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Vinara hukaa ndani, nje kwenda si yakini,
Hawatafiti asilani,wajue vyote viini,
Kwa mtu kutathmini,na taasisi nchini,
Twabahatisha mizani,vipimo viso razini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Asiyeelewa ni nani, nchi ina ukubwa gani,
Kuitawala kitini,au pawe ni mezani,
Huwezi mwana yamini,ni usanii na utani,
Mkoa sio zamani,ni nchi kwa humu ndani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Wenyewe jifundisheni, wakuu elimikeni,
Lugha yetu ni auni, tuanze kuithamini,
Dhana zote za thamani, tuziongelee kwa undani,
KIswahili kwa yakini, ndio dawa ya umaskini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Nani lugha za kigeni, zawa kwao fikrani,
Zinasinyaa na fani, vipaji vyawa laini,
Mawazo ni mgandoni,hatuyajui ya mbeleni,
watu ni shairi guni,haifai kulighani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Rasilimali nuksani,zinawafaa wageni,
Mwenyeji si afueni,atajali kitu gani,
Twazidi mjaza madeni,Kichwani na miguuni,
Atembee namna gani, atoke humu jangwani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Mifumo kitu makini, nafasi sasa ipeni,
Nani hapa duniani,haondoki madarakani,
Mmoja tukimuaminitutaingia mashakani,
Vichaa watatuahini, wakija uongozini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Hii ni yangu imani,na msingi wa amani,
Watu wawezesheni, waukimbie umaskini,
Raia wa kuamini,aliye na kitu tumbuni,
Vinginevyo mwajizaini,yatawatokea puani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

No comments: