Wednesday, September 15, 2010

Mabruki

Nikidhani mamluki, ni watu tu wa vitani,
Hadi nilipohakiki, kama vile ya utani,
Na kuona halaiki, wapo pia mitaani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Wengi hawaaminiki,watumiwa na sultani,
Mambo yao unafiki,wengine huwa shakani,
Yafaa mtaharuki,watawatia matatani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Binadamu hapendeki,hata ukimthamini,
Dhamira yamshtaki,kwa kile anachothamini,
Na daima hatosheki,hadi kwenda kaburini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Utampa ustahiki,vitendoye uzaini,
Mkubwa haheshimiki,pindi awapo gizani,
Na mdogo haaminiki,utapomweka dukani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Wabaya ni marafiki,na wala sio wageni,
Na ndugu hawabebeki,huvunja zote mizani,
Na jirani huwashiki, husuda yawazaini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Mke kwa mme fasiki,si mkweli nje na ndani,
Mme kwa mke fataki,hatosheki na hisani,
Maisha kama hilaki,na nuksi majumbani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Sio kama nahamaki,sina ninachothamini,
Na wanaonidhihaki,si mizizi duniani,
Njia yangu mashariki,magharibi sijabaini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Ayajuaye Khaliki,ya pamba au katani,
Historia kamiliki,kahifadhi ya zamani,
Naye hana mshiriki,ajua ya akheirini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Nafusi haiamaki,yaendayo duniani,
Mimi sio mhakiki,badala siitamani,
Machache nimeafiki,kuyatia matendoni,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Husema sieleweki,na hilo naliamini,
Wajua sitingishiki,chini nashika makini,
Huona sitabiriki,wanalijua yakini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Nyota yangu Mabruki,ahadi sina moyoni,
Hamnao wa laiki,nao hawajabaini,
Hadi azuke Buraki,kunipeleka peponi,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

No comments: