Wednesday, September 15, 2010

Kwa haki au dhuluma

Kiogopeni kiyama, kwa zenu hizo amri,
Mwatenda yenye dhuluma, utadhani makafiri,
Kupunja sasa azma, si mkaaji si msafiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Nusura imeshahama, imebaki tahariri,
Zaja mbegu za nakama, kuzipanda si hiari,
Ni nani wa kulalama, eti ndani kuna kheri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Pastahilipo heshima, pabakia makaburi,
Kwingine kote zahama,kwa kiburi na jeuri,
Ni nani mwenye huruma,watawala waso kheri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ubinafsi wavuma, wavuja sio kadri,
Watoto na wao mama, baba naye adhikiri,
Kabaki peke yatima, maisha yamuathiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ukabila wa kichama, wapashwa kwenye tanuri,
Nchi kuja kuichoma, kama ilivyodhihiri,
Wataimba usalama, huku hali ni hatari,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Na mahala pa heshima, kinyume kinadhihiri,
Pema si tena pema, pameingia ya shari,
Mnyonge sasa agoma,kwake hakunayo kheri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ni nani asiyekwama,katika yake kadiri,
Nafsi zinatuhama,twamuachia Ghaffuri,
Twafunga zetu kalima,twaila yetu shubiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Eneo utalihama, ikishatoka amri,
Fidia hutoifuma, ukipata ni sifuri,
Twenda mbele twenda nyuma, nashindwa hili kariri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Maombi utayatuma, mikopo kutafsiri,
Zitakukweza gharama,na riba bila urari,
Ujenzi utasimama,na benki kukuadhiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Na ukienda kulima, hukukwaza usafiri,
Ukivuna utadema,hasara kukuhasiri,
Utajihisi yatima,kitanzi kukitabiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ajira sasa hujuma,utabakia fakiri,
Zimekimbia neema,madhara yameshamiri,
Tabaka zinakunjama,madaraja si hodari,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Mdhibiti yuko nyuma, jina laalika shari,
Wazibebao tuhuma, mbona hawatiwi kabari,
Nani abebe gharama,maisha kuwa kamari,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

No comments: