Tuesday, September 14, 2010

Karaha za Daladala

Starehe tulopewa, ni mabasi yenye hila,
Mashangingi watumia, walio wetu wakala,
Mtumishi atumikiwa, na bwana kibarakala,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Wasema wanaojua, maisha ya utawala,
Ukitaka kutambua,watawala wa hewala,
Hawawezi kukunjua, njia kuwa mkabala,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Ukishindwa simamia, mitaa na daladala,
Vipi nchi kuiongoa, ikawa ni bora dola ?
Naona mwatutania, nami si mtu wa hawala,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Twashindwa kufurahia, tunapoenda mahala,
Ni mkosi inshakuwa,kuitwa kwenda pahala,
Ni uchungu wa kuzaa, wote tunayo madhila,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Uchungu tunasikia, kugeuzwa ni mafala,
Hadithi twahadithiwa, hatuioni jamala,
Alinacha watwambia, tutapaa Salasala,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Lipi tutalojengewa, na yepi ya mawakala ?
Chini tumeshazidiwa, juu kweli tutalala?
Hii ingekuwa ngekewa, si shilingi ni kwa dola,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Mashimo tumechimbua, hatujaiona hela,
Afadhali ingekuwa,haya yasiwe masuala,
Na nchi ingetembea, badala sasa kulala,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Tumewakabidhi njia, wasioheshimu mila,
Limbukeni wa rupia, watufanya majalala,
Na nchi yaangalia, abiria ng'ombe fala,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

Ustaarabu wapotea, twaishi nayo madhila,
Nani wa kumlilia, nao ndio bwana wa sala,
Twabaki kujiinamia, kumlilia wetu Mola,
Karaha za Daladala, hadi nchi naichukia!

No comments: