Tuesday, September 14, 2010

Wema nilishautenda

Kiumbe mtu wa sanda, ila haishi kudanda,
Wema ukishamtenda,jua huvuni matunda,
Vingine hujamganda,aende anakokwenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Wajibu wangu natenda, japo yapo nisopenda,
Utu wanipa ukanda,na hasa panapo kinda,
Hata kwa wanao pinda,kunyoosha nitakwenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Siondoki na kitanda, achilia hilo banda,
Na wa kumi si wa kenda,dunia sijaipenda,
Kuna ninapopawinda,kwalo hilo najipinda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Kiumbe kama kidonda,harufuye hutopenda,
Akikua hujisunda,ukadhani kawa nunda,
Akawabeza watenda,wema waliomuunda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Mi' na maisha si chanda, njia toauti twenda,
Ningekuwa na kiwanda, siwezi nacho kwenda,
Namshukuru Mkunda, kwa uhai kanipenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Siangalii kalenda, watu hautawapenda,
Utajiponza kwa inda, kwa kuyameza mafunda,
Hali anayekupenda, ubaya hatokutenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Choyo ya anayependa, ni ili uzidi kupenda,
Hasidi si wa kutenda, daima hutaka kushinda,
La kuchanua huvunda,na lijalo pia huenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Mbegu inashinda ganda, kwa thamani na kupenda,
Kwa wengine huyo Honda, mchezaji wa kandanda,
Hali wengine wakonda, na panga lenye kuranda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Pikipiki ipo honda, na Mchina keshaponda,
Taiifa lina maganda, njia yazidi kutanda,
Na wafu watatulinda,makaburi tusipopenda?
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Wema kwangu ni mlenda, si mboga ya Kinywaranda,
Huvutika ukaenda, na tonge linakokwenda,
Na watu sijawaganda,nikawa gundi kuganda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Hali hii naipenda, kusahau nilotenda,
Niepushe nayo Inda,wewe unayenipenda,
Himaya yangu kulinda,kwa yale niliyowatenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

Nichagulie kupenda, kile unachokipenda,
Na kushindwa na kushinda, iwe kwango moja kanda,
Nivaapo yangu sanda, wewe uzidi nipenda,
Wema nilishautenda, acheni nimeze funda.

No comments: