Monday, September 13, 2010

Binadamu ana chaji

Binadamu ana chaji

Binadamu kama smu, kila mtu ana chaji,
Fanya ni kitu azimu, ya mwenzio kuihoji,
Wajibu uufahamu, mwenziwako kumchaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Ni jambo bora na muhimu, kuzijua hizo chaji,
Ili upendo udumu, kwa kutimiza hitaji,
Kwalo uwe mkarimu, huu ni mkubwa mtaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Angalia madhulumu, wasifanze ufujaji,
Kukuuzia wazimu, ilokuwa mbovu chaji,
Haitoongea simu,mawasiliano hayaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.
.

Minara haitodumu, hushuka chini ulaji,
Netiweki huhasimu,hawapati wapigaji,
Na amri husalimu,pakawa ukatikaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Jua aina ya simu, zingine wababaishaji,
Betri ndani sumu, na milele haichaji,
Mwenyewe wajidhulumu, sikuzote upoaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Na ukubwa si muhimu, zingine hazitachaji,
Upya unagharimu,tatizo huwa kuchaji,
Mtumba waweza dumu,kwa umbo pia na chaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Saizi zingine bomu, fanya uchakachaji,
Tafuta kitu kidumu,okoa wako mtaji,
Si ulaini ni ugumu,mtu unaohitaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Bora tena za karibu, za mbali hazifariji,
Hukata bila sababu, pasiwe uongeaji,
Vigumu kuja naibu,pakawa na ufaaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Milki kitu kiamu, kitunze wakihitaji,
Ziangaze zake ramu, uakibishe meseji,
Iweke njema sehemu, kamwe pasipo na maji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Nishati kitu muhimu, ukiikosa huchaji,
Umeme wenye wazimu,huleta ulalamikaji,
Weka na Kobe adumu,aina zote huchaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

Tanesco si karimu, wamezidisha ugwiji,
Waweza kukugharimu,ukose unalohitaji,
Ukajikuta madhulumu,umebeba ufuaji,
Binadamu ana chaji, ing'amue yake chaji.

No comments: