Sunday, September 26, 2010

Hata ukiwa tajiri

Hili nimetafakari, nakuiona shajara,
Wengi limewaadhiri,wanapokwenda zurura,
Wote wakatahayari,waonapo taathira,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Ni wa ovyo ufahari, mtu wa nchi fukara,
Wewe ni mtu wa shari,katika yao hadhira,
Huwa hawafanyi siri,kila kona hukuchora,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Rais au waziri, nyie nyote mafukara,
Lala hoteli mashuhuri,ni mwizi zao fikira,
Panda gari la fahari,trafiki hulipora,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Helikopta safiri, na ndege iwe tiara,
Bado hawakustiri, kwao ungali fukara,
Fanya uwezayo kheri,wewe mtu wa hasara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Wapo wetu matajiri, nje huenda ziara,
Waulize kwa urari, huikunja yao sura,
Wazungu huwaadhiri,wakajiona majura,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Fukara wewe tajiri, nchi yako yasakura,
Kokote ukiabiri,hilo halina stara,
Katika zako safari,jua hili si bishara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Huonekana ghururi,mtu asothaminika,
Thamani yake sifuri, tena hajakamilika,
Mustakabaliwe shari, na hafai kwa ushirika,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Mmoja mmoja kiri, si ukwasi ni ufukara,
Kujionesha ghairi, kwa nyimbo nazo bendera,
Ili uyatafakari,watu wako wote bara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Uchumi uwe mzuri, tubadili yetu dira,
Wote tukiwa kwenye heri, twaweza kuuza sura,
Vinginevyo minghairi,yakini kwenye ubora,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Ulaya sina safari, wanihini ufukara,
Pia sinayo habari,Marekani kuzurura,
Sijaona alfajiri,nachelea ufukara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Ninamuomba Bashiri, kutupatia nusura,
Waache kutuhadhiri, sisi tunaodorora,
Tupate wenye akheri, kuwa ni wetu vinara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

No comments: