Wednesday, September 15, 2010

Mashairi yanasema

1.
Mashairi yanasema, mengi yanatuambia,
Kwa watu wenye hekima, kauli huzizingatia,
Na palipo waadhama, waidha huzingatia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
2.
Yashangaza hizi zama, kuipuuza sanaa,
Zunguka nchi nzima, ushairi unapwaya,
Nai zinazorindima, adili zadidimia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
3.
Shuleni wameshakwama, nani kutunga ajua,
Afundishaye ni ndama, ng'ombe wameshapotea,
Kukamua wamekwama, upepo wawapepea,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
4.
Redioni wamehama, watunzi waliokua,
Sasa zimebaki ngoma, na makelele kufua,
Halfani hana hema, baridi augulia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
5.
Andanenga kasimama, gumzoni kaingia,
Utunzi kaona noma, maslahi yasinyaa,
Wala hapana heshima, wala wa kutuangalia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
6.
Ninatweta, ninahema, hili sikulitegemea,
Nchi yenye takrima, utunzi isiyowafaa,
Watu wafunga kalima, busara kuyoyomea?
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
7.
Kitu gani anasema, Shaaban alipokua,
Mnyampala muadhama, hili hakulifikiria,
Shehe Abedi daima, asingelitegemea,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
8.
Mochiwa kabaki nyuma, hadi anajiondokea,
Mla mbovu kainama, hili hakulisikia,
Abdulatifu kahama, Uingereza kaselea,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
9.
Kiswahili kitazama, bila utunzi kukua,
Wasiokitakia mema, hawataki kukitumia,
Vyuoni wanakilima, eti sio maridhia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
10.
Elimu imesimama, tena yazidi sinyaa,
Kiswahili kukinyima, ruksa kufundishia,
Ni kweli mkataa pema, panakomwita pabaya,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
11.
Mitume wametuhama, lugha yetu kuiua,
Tambiko zimegangama, hakuna wa kutusikia,
Na midomo imeachama, twadhani twaomba dua,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
12.
Mushawari kagoma, uzuri umepotea,
Sasa twaicheza ngoma, asili tusioijua,
Akili zimetuhama, tumebaki kubabia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
13.
Mashairi yanasema, viziwi watasikia,
Makilla akilalama, wengi watamsaidia,
Ni tamu lugha ya mama, utumwa nyingine kua,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
14.
Semeni mliosoma, Mlokozi chokonoa,
Kahigi tia kalima,na vijana mlioingia,
Nchi yataka neema, ije vipi bila lugha?
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!

No comments: