Wednesday, September 15, 2010

MCHWA

Siku ya kuangamia, mchwa huifurahia,
Mbawa atazawadiwa,na angani akakwea,
Huku na huku kupaa, aranderande na njia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Mwenyewe hufurahia,mbumbumbu bila kujua,
Mauti yamngojea, njiani asikojua,
Ghafla hushtukia, Ziraili amchukua,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Haya ndiyo ya dunia, na jinsi inavyokua,
Uombacho utapewa, ovyo au cha kukufaa,
Na vingine mwajaliwa, ajali kuwaletea,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Laiti ungelijua, gari usingepokea,
Kwamba laja kukuua, na siku hazijafikia,
Na nyumba usingekaa, kama waja kuvamia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Mafuu hufurahia, pasipo kuomba dua,
Mwenyewe akiaminia, uwezo wake wazua,
Neema hujichotea,shukrani kuzuia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Muumba yote ajua,na riziki huzigawa,
Hachagui kama mbaya,au anayemnyenyekea,
Wote atawapatia,mbaya kumzidishia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Viumbe huwashangaa,kumnyima japo dua,
Ila hatopungukiwa,hata bilioni mkiwa,
Wangali wanaojua,wao wamhitajia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Heri wasiojaliwa, hawana la kulijutia,
Mwepesi wauchukuam mzigo walokabidhiwa,
Na deni lao walijua, sio la kuwashadidia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Wale wanaojaliwa, hisani kutotambua,
Gogo watalichukua, chini likawashindilia,
Hapana wa kuwanyanyua, siku itakapoingia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Cha heri kilichokuwa, motoni huja watia,
Duniani huanzia,masahibu kuwavaa,
Wengi huchanganyikiwa,baadhi kuwa vichaa,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Katu sintoajabia, wazuzukao jamaa,
Kwingine hawajajua,na hawajaangalia,
Pepo zinakoendea,na misimu tarajiwa,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Siku ya kuangamia, mchwa hushangilia,
Mabawa anayopewa,hayeshi kumzuzua,
Huruka na kuingia,kwenye taa kujifia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

No comments: