Tuesday, September 14, 2010

Barabara jahanamu

Salamu za Jahanamu, zimenichosha ubongo,
Zasema watakadamu, wao hawajui hongo,
Barabara zao amu,zazidi zetu za Bongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Moto ni yao salamu,ila hamna uongo,
Wajenga kitu cha hamu,kukaa tena miongo,
Na kila mja kwa zamu,hujua la kwake pango,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Wenyewe twajihujumu,wakazi wa hapa Bongo,
Tumekuwa wadhulumu,hata nafsi misongo,
Hatuna lililo adhimu,tumejaa makorongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Barabara Jahanamu,bora kuliko za Bongo,
Kidogo zinagharimu,na wala si za udongo,
Wahandisi wahitimu,kengeza haliwi chongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Kumbe bora kuzimu,kuliko kuishi Bongo,
Hii ni mbaya hukumu,viongozi wana zongo,
Nafsi hazijilaumu,maisha yao urongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Maisha yetu ni sumu,na wakuu wetu gongo,
Siasa zao chandimu, ukarimu wao mbungo,
Wananyonya mawe damu,mali asili viungo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Mikataba ya wazimu, wazungu wawapa hongo,
Ujenzi wamekasimu, hawauwezi Wabongo ?
Vipi tutatakadamu, bila kujenga Wabongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Nchi bila gurudumu, ndio yetu hii Bongo,
Twaburuzwa kihaskumu, si ikulu si wa mjengo,
twashindwa kuwahukumu, bado tuna tongotongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

Wameisha binadamu, twazaliana mafungo,
Halali kwetu haramu, na haramu ni mchango,
Umeisha ukarimu, twapigana mazongo,
Barabara Jahanamu, bora kuliko za Bongo.

No comments: