Tuesday, September 14, 2010

Jambia langu upendo

Siichelei mizinga, silaha yako upendo,
Sijali jeshi la anga, kwangu kama kitu mgando,
Meli zilizo na kinga, kwangu zitapita kando,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Hapa nimetia nanga, naweka wangu utando,
Ajaye namchabanga,ni bora apite kando,
Usijitoe mhanga,utageuka uvundo,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Vita nilishaviunga,mambo yafata mkondo,
Adui nilishawazonga,hawana mbinu miundo,
Wanatumia mapanga,enzi za makomandoo,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Ukidhani ninavunga, njoo na chako kimundo,
Nitaachia wachanga, watakupigilia nyundo,
Kisha lije tingatinga,likutupilie kando,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Usijepiga masanga, ukajiona mchundo,
Kitali chataka konga,mbilimbi navyo vifundo,
Akili kama upanga,kuyaratibu matendo,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Tambo hizi ninaringa,malenga mfuzu jando,
Kutunga kwangu kupanga, na maneno yangu mdundo,
Wengine wanajivunga,huu si wao mwenendo,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Mafisadi wana kinga, kazi zao za magendo,
Binafsi najichunga, sitaki la kwao windo,
Kiama chao chachonga,akili kuwa mgando,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Huba na hawa charanga, msitishike na nondo,
Malenga wetu atunga, nyuklia zenye mwendo,
Na nyoyo zetu akonga,hadi kwenye yake mapindo,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

Kasri ninaifunga, umetosha huu mwendo,
Kambi hapa naipanga,nangoja kina msondo,
Na majini nawaganga,wakae kwenye langu lindo,
Jambia langu upendo, dunia nitaishinda.

No comments: