Wednesday, September 15, 2010

Mkuu wa wilaya mambo ?

1.
Wilaya inaugua, hili ndugu walijua,
Tabibu anatakiwa, wilaya kupata dawa,
Wote mnajifungia, ofisini mnasinzia,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
2.
Maendeleo vitendo, lazima kuyapangia,
Mengine wekeni kando, kwanza muonyeshe njia,
Hayo mawazo ya mgando, zamani tumeshakataa,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
3.
Wilaya ina ardhi, tupange cha kuzalisha,
Na jinsi ya kuhifadhi, tija tukaizungusha,
Wilaya ipande hadhi, na kujitofautisha,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
4.
Wilaya ina madini, vipi lije tumaini,
Utoke umaskini, watu kukosa thamani,
Tuipate afuteni, vijijini na mjini,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
5.
Wilaya ina maziwa, vipi tuyapate maji,
Ili yaweze kutumiwa, na kuwa ni wetu mtaji,
Mashamba kunyeshea, tukafanya uvunaji,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
6.
Wilaya ina mifugo, tuwafuge namna gani,
Wasiwe kwetu mzigo, bali amana makini,
Na sisi tuwe vigogo, Mbeya na umasaini,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
7.
Wilaya ina asali, vipi mbaya yetu hali,
Tunazo na pilipili, mbona maisha shubili,
Twala na kusaza wali, ila hatuna afadhali,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
8.
Nini chanzo cha tatizo, lazima tupate jua,
Utafiti mzomzo, lazima kujifanyia,
Tupate maelekezo, njia ipi kutumia,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
9.
Wengi wasema nchini, sisi mbona matajiri,
Hatunao tu umakini, ndio twawa mafakiri,
Ili tuwe sio duni, tuianze mpya ari,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
10.
Wilaya sio ngomani, wilaya ni kampuni,
Meneja watafuteni, miradi waje baini,
Mipango nayo wabuni, kwa mkubwa umakini,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
11.
Wialay ni kampuni, viranja badilikeni,
Urari uwe juani,wala sio mafichoni,
Nini wilaya thamani, na wapi mlipo duni,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
12.
Amali zenu jueni, hizo ni hisa yakini,
Watu waelimisheni, kwa KIswahili laini,
Wasoenda darasani, nao pia watamani,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
13.
Ukuu sio masuti, wala fashioni mpya,
Huo ni uzumbukuti, mafiga hayana chafya,
Wananchi ndio yakuti, wataka moyo kulea,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
14.
Ukubwa sio ofisi, fenicha nalo gari,
Ukuu si kutanafusi, wala njaa ya fahari,
Uongozi uasisi, heri ya wote si shari,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?

No comments: