Sunday, September 26, 2010

Hii bado Afrika

Wazungu wanayopika, kwetu vigumu kulika,
Ila njaa imetushika, sasa tunalazimika,
Na mwishowe tutatapika, na hapa hapatakalika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Dini sisi tumeshika, twaogopa kulanika,
Hicho wanachokitaka, Ulaya na Amerika,
Yafaa kueleweka, kisiivuke mipaka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Paspoti ya kuvuka, isiwe kwa yao sadaka,
Utamaduni hakika, wetu umeshajengeka,
Ukija kuporomoka, mabaya yatatufika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mwanamme hajaposeka, achia kuoleweka
Na dini zinatutaka, hili kutokubalika,
Huo wao ufuska, tusije shawishika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mwanamme Afrika, yake yanaeleweka,
Kisha hali kadhalika, mwanamke aitika,
Na ndani kuna mipaka, majukumu kuyashika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Biblia yasomeka, na haya yatambulika,
Kurani yanatajika, muumini waridhika,
Ila wanaohangaika, wa wazungu vibaraka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mapinduzi twayataka, sio ya nguo kuzuka,
Ustawi twautaka, sio wa kuvurugika,
Usawa una mipaka, kwingine huwezi fika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mke wangu namshika, na wote tunanyanyuka,
Mipaka hajaivuka, na kwangu aheshimika,
Na simba hajawa paka, mwisho panya kugeuka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Hii bado Afrika, Wazungu ninatamka,
Yenu yasiyoeleweka, huko huko mgeshika,
Hamnayo madaraka, kutuuzia talaka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Ulaya mlisifika, kwa wake kunyanyasika,
Mkawata kwa mashoka, mashgoa waliozuka.
Na sio mingi miaka, hili linatambulika
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Nafasi tunaitaka, na ya kwetu kupangika,
Mwajua tunayoyataka, unyonyaji kufutika,
Na malengo ya kuvuka, ufukara kufutika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mengine yatafikika, taratibu tukitaka,
Hatua zitavukika, hadi malengo kufika,
Iamue Afrika, si nyie kuamulika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

No comments: