Tuesday, September 14, 2010

Nilipoibusu dunia

Haya kamwe sikujua, siku nilipoingia,
Jinsi walivyonipokea, malaika nilidhani,
Miaka ilivyosongea, wote wamenibadilikia,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Pepo niliidhania, nilipobusu dunia,
Bashasha iliyojaa,na juu kuninyanyua,
Wemgi kuniangalia,na mengi kusingizia,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Shilingi kunichangia, na zawadi kuniletea,
Mabusu niliyopewa, mfalme hajajua,
Dua wanakanisomea,za uzima na afya,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Pati ziliandaliwa, wakaalikwa maridhia,
Dansi wakaitimua,hadi machweo kuingia,
Vyakula vikagawiwa,na vinywaji vikanyewa,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Mara nilipobakia, na karibu walokua,
Wageni wakapungua, hadi wakaishiiia,
Zaidi nilichosikia,ni buta na kubutua,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Na joto likaingia, hari ikawa tabia,
Marashi yakapungua, harufu kuwa kinyaa,
Na rangi zikafifia, nzee nzee zikawa,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Mwezi ukanizomea, badala ya kunishangaa,
Nayo miale ya jua,ikageuka mkaa,
Na upepo ukakua,hadi kimbunga kikawa,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

Machozi sikuyajua, japo najua kulia,
Baridi sikuzoeya, hadi nilipotambaa,
Na shida sikuzijua, hadi mtu nilipokuwa,
Nilipoibusu dunia, pepo niliidhania!

No comments: