Tuesday, September 14, 2010

Tanzania twala sumu

Si sukari si mafuta, naona nalishwa sumu,
Pamoja na huu ukata, yanazidi madhulumu,
Ni wapi nitampata, asiye mwana haramu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Utafiti umetota, idara hazina hamu,
Wapima pasipo mita, utapataje takwimu,
Na njaa inatusuta, wengine kulisha sumu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Hili lataka kuteta, na jopo la wala sumu,
Kila mmoja atweta, kutafuta mdhalimu,
Ingawa njiani twapita, wengine si binadamu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Sukari yameremeta, lakini ndani ni sumu,
Chai unapoipata, yaenda chafua damu,
Viungo hukatakata, na kukutia wazimu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Mafuta wanayoleta, hayafai wanadamu,
Mwilini yanatokota, japo chakula kitamu,
Miili inateketa, na nguvu zinahsimu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Viongozi wanapeta, nyumbani hawali sumu,
Je, hotelini wakipita, hawaipati salamu,
Adhaniaye apepeta, aweza kuwa mdimu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Waume watukeketa, nyumba zinakuwa ngumu,
Vuta nikuvute vita, wali wakitahamimu,
Kazi nyumbani twaleta, chumbani kutokudumu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Viongozi twatafuta, wa kikosi maalumu,
Kuyachekecha mafuta, yaliyojaa haramu,
Madukani wakapita, kuyafanyia hukumu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

Usukani wamevuta, kweli watu gurudumu,
Na mkia wanafyata, kwa uzito na ugumu,
Na muda ukishapita, huchomwa nayo kaumu,
Tanzania twala sumu, na rijali si rijali !

No comments: