Tuesday, September 14, 2010

Udugu maridhiano

Kura ya rai agano, yaleta maelewano,
Pamoja na mashindano, wote vidole vitano,
Twataka utangamano, na sio mavurugano,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Udugu ni maridhiano, tena kubwa fungamano,
Na mkono kwa mkono, umoja na mivutano,
Hatima ni moja neno, nchi ipate vinono,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Sasa yaja mashindano, wala si tena ndoano,
Yaisha matafutano, sasa twataka mifano,
Watu wapate mavuno, hasara iwe ni ngano,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Vyama viwe ni mikono, ya kuleta uwiano,
Kisha na mapokezano, uchumi uwe mnono,
Dawa ya mfarakano, shibe iwe makutano,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Visiwa viwe mfano, kwa vitendo si maneno,
Yemeni hadi Ureno, wakumbuke zama hino,
China na India wino, waweke ushirikiano,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Yawepo makongamano, mawazo kuyapa neno,
Tuache shika kiuno, tuifanye changamano,
Na hatutaki miguno, hao tuwape kisigino,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Mseto na uwiano, ndio la kwetu agano,
Nafasi kwa mashindano, washinde wenye maono,
Wa usingizi wa pono, tuwaache kwenye vono,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Kazi kwa mazinduano, si kubweka bila meno,
Shuruti si uwiano, bali hali mazidiano,
Na bongo za misumeno, ndizo tutakazo hino,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Mwendo uwe mchuano, kuleta yenye machano,
Pasiwe na konokono, wala kobe mgandano,
Nchi yataka mashono, shehena msongamano,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

Yaenziwe maridhiano, mseto na uwiano,
Nchi ipate tangamano, na fanaka mlingano,
Maadui ni kibano, waiza maelewano,
Udugu maridhiano, mseto na uwiano.

No comments: