Saturday, September 18, 2010

Pensheni zinaliwa

Tofauti sijajua, ya hisa na kuchangia,
Makato ninayotoa, ni fungu nawekezea,
Bado mnaniambia, mwanachama nimekuwa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Kazi najitegemea, changu mnakichukua,
Kasri mwajijengea,kibanda sijakijua,
Nishai mnanitoa,wezi ninawafikiria,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Hata ninapougua, juzi ndo mwagundua,
Huduma nahitajia, na lazima kulipia,
Zama hivyo haikuwa, mwenyewe mliniachia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Ada zinanisumbua, kunikopa mwakataa,
Uchungu ninaosikia,kama vile ninazaa,
Nataka kuwafunua,kisha nikawafukia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Kinachostahli kuwa, nilichokinunua,
Vipi mnakiachia, walaji kusimamia,
Meneja sijamchagua,na wala sijamjua,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Ukiritimba mwakaa, yote mnajivutia,
Naona sasa yafaa, unyonywaji kukataa,
Pensheni kuachia,ziwe za waajiriwa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Serikali inafaa, pembeni kuja kukaa,
Nyingine kufungua, binafsi kwa ridhaa,
Ushindani kuingia,pasiwe anayesinzia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Pensheni maridhia, mmiliki humfaa,
Hisa anazozitoa, kampuni yake huwa,
Hakuna wa kuingilia,maamuzi anayotoa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Kwa hali ilivyokuwa, mmiliki atwibia,
Siye wa kumkubalia, huyu anatuingilia,
Maamuzi anayotoa,hayawezi kutufaa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Amkeni Watanzania, hivi sasa twaibiwa,
Ufukara tutaoa,ndoa isiyokataliwa,
Watukaanga wazawa, samli yetu watumia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Inabidi kushupaa, cha kwetu kukichukua,
Najua watakataa, nasi tutawakatalia,
Lazima kuwapakua, tupike kinachofaa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Copyright © Sammy Makilla-2010

No comments: