Tuesday, September 14, 2010

Sioni maendeleo

Pengine mimi kipofu, maendeleo sioni,
Wasomi wataarifu, mambo kwa sasa makini,
Dola ya jana elfu, ya leo thamani gani ?
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Irejee hiyo brifu, waziri alosaini,
Uchumi kuwa barafu, umepoa frizani,
Nasi tulio dhaifu, utaisha walakini,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Magunia ya sarafu, hayanunui gauni,
Nauli za maelfu, na umeme mtihani,
Ughali ni msahafu, wakaa serikalini,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Mashangingi manadhifu, kweli yako mitaani,
Hii sidhani sharafu, kwangu huu uzaini,
Chazidi kichefuchefu, njiani na mitaani,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Nchi haina wakfu, kusaidia maskini,
Tunashndia madafu, na mihogo vijiweni,
Navyo bei sasa bifu, na pengine huioni,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Twaishi kwenye maghofu, kama sio viotani,
Hawajui watukufu, nyumba sicho cha hisani,
Kasri zao zakifu, huku twafa manyasini,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Afya zetu hafifu, budi tutoe ilani,
Hili la kupigia dufu, wayajue wahaini,
Wanaovaa utukufu, kumbe ndani hayawani,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Sharifu kaniarifu, dua yaleta auni,
Ukweli utasadifu, kwanini neema sioni,
Na zafa safu kwa safu, tutapita mitaani,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Mganga kanikashifu, kwanini bado sioni,
Magari tena maelfu, folenini yamo njiani,
Na pikipiki tramfu,zaranda barabarani,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

Nao kina Eniesiesifu, wajenga mpaka mbinguni,
Maghorofa yatakifu, hamu ya nuru machoni,
Japo kwa njaa dhaifu, huipata afueni,
Sioni maendeleo, pengine mimi kipofu.

No comments: