Wednesday, September 15, 2010

Vuvuzela si mmbeya

Si wanawake wambeya, bali wenye mambo mia,
Pumzi wasiotua, habari kukushushia,
Na kuroroma tabia, na hasa ukiishiwa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela domokaya, hajui la kuchagua,
Na atazungumzia, hata asiolijua,
Na ubishi huvamia, bila asili kujua,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Maneno kama mvua, isiyokubali jua,
Kisima chake hujaa, japo siyo yanayofaa,
Mdomo kuufunua, kama saluti kutoa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Hakuna asilojua, Vuvuzela nakwambia,
Na mengine huyazua,matope akakupakaa,
Ni mtu wa kuhurumia,kwa maneno ni kichaa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Haachi kuyarukia, kila analosikia,
Nguo aweza kuvua, hadharani kwa butwaa,
Ni mwenye kujisifia, japo hajajiangalia,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela litalia, hata usipokosea,
Lawama huwa lazua, wakati lafadhiliwa,
Ushindi kuuchukua, muhali haijatokea,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela linalia, kipato kikipungua,
Kitu aking'ang'ania,kama usipompatia,
Utakesha waimbiwa,lepe hutolitambua,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Umbeya akiletewa, hawezi akachungua,
Vuvuzela litalia, jirani wakalisikia,
Na machozi litatoa, eti kwamba laonewa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela ni mkia, kichwa ni nadra kuwa,
Sapoti huweza toa,pale pasipotegemewa,
Matatani ukaingia,usijue pakutokea,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela hutimua, ndugu na pia jamaa,
Kwa kelele kuzidia,hadi wakachanganyikiwa,
Hamna wa kulisifia, "Arsenal' walikataa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Mpira ukiangalia, kulala litakwambia,
Ukitaka kutembea,sababu litaizua,
Kwanini leo yafaa,nyumbani ukabakia,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Kama ulishachagua, Vuvuzela kununua,
Na nyumbani limejaa,basi ndugu vumilia,
Hatima yako ngojea,ya taabu na udhia,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

No comments: