Monday, September 13, 2010

Kilichobakia

Ikitawala hadaa, na uongo kuenea,
Haki ikinunuliwa, na dhuluma kuzagaa,
Zinaa juu ikiwa, fikra chini kukaa,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Dharau ikichanua, na kufuru kuvimbiwa,
Jeuri ikishangiliwa, na kiburi kikikomaa,
Magari yakiheshimiwa, na mali kuthaminiwa,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Wezi wanaposimamia, nchi kwa kuchaguliwa,
Na ukuu wakachukua, na wenyewe kujiibia,
Wizi ukakubaliwa, na wezi kuabudiwa,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Ubinafsi kijaa, wakizidi wenye njaa,
Zinapohasiri mvua, badala ya manufaa,
Mikosi yenye balaa, kawaida inapokuwa,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Linapokengeuka jua, na hari kutapakaa,
Yaeneapo mafua, na magonjwa ya kifua,
Watu wasipojitambua, usalama kupotea,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Wengine wanaposambaa, na mbali wakahamia,
Marafiki wakivia, na ndugu kukubagua,
Upweke ukiingia, na pekee kubakia,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Siku unapoishiwa, hunacho cha kutumia,
Jangwani unapokuwa, na umekwishachanganyikiwa,
Huna unalolitegemea, wala pa kukimbilia,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Mola anaposikia, na majibu kuyatoa,
Hasira yake kutoa, sunami kufurumua,
Na maji yanaposambaa, na watu kuanza kuua,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Imani inaporejea, na dua kukubaliwa,
Asante ukiambiwa, na shukrani kutoa,
Uhai ukipepea, na maua kuchanua,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Moyo unapofungua, na macho yako kutua,
Mwenzio akiingia, nyuso kaikunjua,
Mikono ikiitikia, naye kukumbatia,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Yote unapoyakataa, na kuyaona udhia,
Unapoachia dunia, iende na yake njia,
Nyuma unapobakia, kama kondoo kushangaa,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Pendo linapochipua, na ndoto kweli ikawa,
Hawa inapoingia, mzima tena ukawa,
Kipya ukakitumia, na hamu kuridhia,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

Pamoja mnapokuwa, kibanda cha kuzawadiwa,
Na mlenda na dagaa,wawili tutabugia,
Ukiangaza mshumaa,mkabala tumekaa,
Kitu kilichobakia, ni rafiki mwaminiwa.

No comments: