Tuesday, September 14, 2010

Treni zetu zina Mganga

Wengine walipeana, yuko wa kweli mganga,
Twamjua ni Mchina, treni anayeganga,
Tukijenga muamana, hata za stima aunga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Wahindi tumeshawakana, hatujui walichohonga,
Hawakuwa na amana, mkengeni tumegonga,
Hili sasa ni bayana, tusiwe tena wajinga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Wasanii twawakana, hawawezi kutuvunga,
China muwape amana, reli zote watajenga,
Madini wapeni sana, kadri wanavyotukonga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Tuache kujitafuna, na kauli kujigonga,
Kama akili hatuna, basi tuwekeni tanga,
Aibu kujishebedua, hamna mnalo panga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Mafundi waliosana, reli walishaijenga,
Nao haya wanaona, ila twawaona wanga,
Na ni vigumu kubishana, tutaonana wajinga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Nchi yataka amana, na mambo yetu kupanga,
Hali yetu itafana,na mengi tutayachanga,
Watu bora kutuona, nasi tukawa twaringa,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Karne hii ya wana, wenyewe budi kujenga,
Teknolojia kuchuna, nasi tuwe wa kujenga,
Mengine kuazimana, hadi angani kutinga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Kusoma twasoma sana, sasa tuanze kujenga,
Vyeti viwe vya amana, mtu awezapo kupanga,
Kisha akalinuia, jambo nalo kuganga,
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

Subira muda hatuna, wenyewe twajikaanga,
Tuache kutaniana, kwa mizengwe na uhanga,
Kizazi kimeshonana, twawakubali wajinga ?
Daktari yuko China, treni zetu zina mganga.

No comments: