Wednesday, September 15, 2010

sagesage hasira

Moyo wazidi kufura, kwa unayonitendeya,
Imetawala hasira,na kutoweka sheria,
Pasipokuwa nusura,mtu ataangamia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Umenifanya ni chura,bwawa ni yangu dunia,
Na mimi ninakuchora,wewe mjanja wajua,
Tarehi ikisowera,tajiju na kujijua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kila nikikupa kura,ndiyo wazidi udhia,
Mnaniuzia sura,mnaniachia njaa,
Mwanipamba kwa bendera,shuka siwezi nunua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Mali asili mwapora,wageni mwawatunukia,
Ardhi mwaisakura,wakuja mnawaachia,
Na hii mbaya bishara,kizazi kinachofatia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Madini mmechakura,hongo mkazipokea,
Tunachokipata hasara,na mashimo kubakia,
Mabepari wanafura,nazidi kujikondea,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Weupe kama sungura,ujanja wamezidia,
Wasiosoma majura,nao mnawapokea,
Mashirika yadorora,kisa hamjakijua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kuendelea ibura,mzawa mkimuonea,
Kama hanayo tijara,nchi itadidimia,
Mkiikosa busara,tutazidi kuumia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kunazo sheria bora,na sheria za mabaa,
Nuksi zenye kukera,hutupa wanaojua,
Ndizo zizuazo hasira,tena na kubwa balaa,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Benki mnazipora,na hifadhi nazo pia,
Uchumi unadorora,wafana mnatwambia,
Zinakwisha barabara,mwanena tunaendelea,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kwa ukubwa nchi mkwara,mikoa mwang'ang'ania,
Madaraka yamegura,hakuna wa kusimamia,
RC ni hasara, watu hawajamchagua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

RC si busara, gavana twahitajia,
Mipango wataochora, mikoa kuendelea,
Nchi kubadilika sura, itutambue dunia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kenya sio masihara, wana katiba mpya,
Sisi tunaodorora,wa kwanza tulishakuwa,
Kuwa na watu kachara, matende yakazuia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Lugha yetu yadorora,zingine twazitumia,
Japo twajua fikra,mizizi zimekataa,
Mataifa yalo bora,lugha zao yatumia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kwa kila kitu twadorora, hatuna tunalong'aa,
Ila tu kwa kujipara,nje wanatushangaa,
Mwendo nyuma zetu sera, masikini twabakia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.


Ninaomba maghufira, Jalali kutuhurumia,
Tunshaipoteza dira,hatujui yetu njia,
Unapotea msafara,jangwani tulipokua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

No comments: