Saturday, September 18, 2010

EITIEMU

Eitiemu imegoma, fedha sijazichukua,
Mfukoni nimekwama,na shida sijaatatua,
Na mtu wa kuazima,bado sijamfikiria,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Kujiamini nasema, leo kumeniumbua,
Sikuwa nayo tuhuma, ndarahima sintotoa,
Kutoka utu uzima, utotoni nikaloa,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Eitiemu kwa heshima, yote nilikupatia,
Nikidhani kwa nakama, sasa nimezikimbia,
Na hulka ya kuazima, mbali nimetupilia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Ndugu nilishawahama, mbali nao nikakaa,
Rafiki nikawasema, mbele wakatangulia,
Eitiemu muadhama, wawili tukabakia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Na kila nikikutuma, haraka ulikimbia,
Ukarejesha uzima, pale ulipopotea,
Ukaniwia karama, kidogo kuabudiwa,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Umbo lako dogo jema, mfukoni waingia,
Mororo ukitazama, na laini ulokuwa,
Ila mkubwa kwa gharama, haja zangu kutimia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Kwangu ikawa rehema, kwa jua pia mvua,
Kila nikikutazama, nazidi kujiaminia,
Daima nikikusoma, na kukuchungulia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Haukunikwaza mtima,nikajua wanijua,
Wewe kwangu ni salama, na kweli nimeridhia,
Ukafanya kila hima, mimi kunitumikia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Ghafla leo nakwama, sijui pakukimbilia,
Imeondoka adhama, mengi natuhumiwa,
Mimi niliyesimama,watu wakashangilia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Mimi niliyesimama, watu wakafurahia,
Leo nahofu hasama,wasijenishambulia,
Ninaifunga kalima, mafichoni kurejea,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Copyright © Sammy Makilla-2010

No comments: