Tuesday, September 14, 2010

Mwenye shibe

Mwenye shibe kakinai, amjuaje mwenye njaa ?
Yeye alikwishawahi, kunawa na kujimegea,
Sasa kama makuruhi, wengine hatowafaa,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Uafrika nishai, kizazi kimelaniwa,
Walipoacha wasihi, wa kutojilimbikizia,
Sasa wote makarai, na kujaa hawatojaa,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Masikini ajidai, eti hadi nje ang'aa,
Wazungu wamstahi, haweshi kumshangaa,
Nyumbani kapa uhai, Ulaya mwajatembea?
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Staftahi hawajui, na cha mchana ni jua,
Meno nje wafurahi, milo mitatu yatua,
Maaluni humtambui, ila kwa yake tabia,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Wameifunga nikahi, na wezi kutuibia,
Wapendeza kwa wajihi, ndani utawachukia,
Na hili haliwasumbui,si watu wa kujitambua,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Mwenye shibe matlai, magharibi ina njaa,
Pepo hawazitambui,na ishara za hadaa,
Wache leo wafurahi, kesho watu wa kulia,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Hawa watu wa nizai, hai watunyanyapaa,
Maiti zao sijui, zanuka au zanukiya,
Kavcaani wa kikoi, kuvaa mbwani kuvaa?
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Hawaisikii rai, wala si wa kuambiwa,
Hawaambiliki sui,ni watu wa kujihadaa,
Wakishakamua tui, dafu haitowafaa,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Kadri yataka kinai, na kiasi si kujaa,
Nani hajitambui, tumbo lake likijaa ?
Ndoo haiwi karai, humwagika yakijaa,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

Salamu na baibai, kwao huwa ni mamoya,
Najua au sijui, kwao maneno sawia,
Sanaa si usanii, na ujinga si ujuha,
Mwenye shibe hamjui, asilani mwenye njaa!

No comments: