Wednesday, September 15, 2010

Mbuyu uangukapo

Ardhi hutikisika,mbuyu ukianguka,
Hadi mbali husikika, watu kote wakastuka,
Huuliza na kumaka, ni nini kimefanyika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.


Mbuyu mti wa hakika, umbo lake lasifika,
Hudhani umegeuka, matawi juu kuwekwa,
Majani yake ya shaka,mizizi huhadaika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Mti umerehemeka, kwa kina umejengeka,
Na wengi huogopeka, eti mizimu waweka,
Watu huwa na wahaka, usiku unapofika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Mti unaabudika, kwa wale wenye shirika,
Matambiko hufanyika, mizimu kubembelezeka,
Kwa kafara na sadaka,madhabahu hujengeka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Ukishika umeshika, katu hautaterereka,
Hana vuli na masika, kote unaneemeka,
Na mabuyu huzalika, watoto wanayoyataka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Upepo huamanika,kuangusha ukitaka,
Kiuno utajishika,na kwenda kupumzika,
Na pumzi zitaushuka,nguvu bure kuharibika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Amejalia Rabuka, na watu ni kadhalika,
Wajao kurehemeka, kwa nguvu kuneemeka,
Au mali kujashika, kwa hali kutakatika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Kama mbuyu hujazuka, wakawa na patashika,
Hawataki kushindika,wala kuja kukwazika,
Watazua hekaheka,tufani nazo gharika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Ukubwa watautaka, wengine kunyanyasika,
Viumbe kudhalilika, wao ndio hufurahika,
Jeuri watapeleka,hata kwaye mtukuka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Ujibari hujivika, wasiwe nao wahaka,
Vioja huibuka, kama Amin mtajika,
Na siku inapofika, mbuyu utaanguka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Jibari atadondoka, wasifu kuporomoka,
Hakuna atalodaka, ila wingi wa mashaka,
Dunia humgeuka, na kujiona kichaka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

No comments: