Tuesday, September 14, 2010

Tubaituu

Mashaka yanikomaza, na hasa muongo huu,
Yamezidi makomaza, utadhani vichuguu,
Nashindwa mate kumeza, uchungu kama tambuu,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Motokaa zatukweza, tuendao kwa mguu,
Pikipiki mwatandaza, kulemaza vitukuu,
Akili kama zaoza, hatujui vya nafuu?
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Tumeshindwa kueneza, barabara za tanuu,
Sasa tunajiagiza, kujenga za juu kwa juu,
Nchi inakerekeza, njia zake kuukuu,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Akili tumelemaza, utadhani ni mafuu,
Mbele yetu kuna kiza, waongoza vipofuu,
Mabovu twajipongeza, bora tumeshasahau,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Hali inatutatiza, na kwetu sio ishuu,
Mambo yanatushangaza, zavurugika juzuu,
Vioja twaviangaza, wa chini kuwa wajuu,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Raia usipomkweza, nani awe sasa juu,
Vyombo mmeviagiza, viwe ndio wetu wakuu?
Twaabudu vya kupoteza, vya kuenzi twadharau?
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Pikipiki twatukuza, sio mwenda kwa mguu,
Vivuko kuvikatiza, twaogopa mbaumbau,
Taa zikitukonyeza, hatujui letu dau,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Twabakia kuapiza, kwa laana na malau,
Muumba kuwatekeza, wasiotupa nafuu,
Na ari twaipoteza, kwa nchi ya vigeugeu,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Imani tumeichakaza, imeisha sikukuu,
Wananchi twawachukiza, hawawaombei kwa Afuu,
Na kilio watakitangaza, pengine mpate ngeu,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Enzi anayeeneza, muumba wake Samau,
Vita akija tangaza, vitaoza vitunguu,
Na macho kuwa kengeza, kwa kutufanya mazuzuu,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

Njiani mnanikimbiza, nipite wapi tubaituu,
Au nami juu naweza, kutembea mwaka huu,
Nikaelea mwangaza, washangae mabahau,
Nauliza wenye nchi, nipite wapi tubaituu.

No comments: