Wednesday, September 15, 2010

Yafute haya machozi

Umeshanipa simanzi, tena kwa mingi miaka,
Hali hata huulizi,kwako nimekwishazikika,
Kwa hii yako ajizi,vibaya nimeathirika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Sijayajua mapenzi, ila ni kuhangaika,
Ingelikuwa maradhi, kwa kweli ningeponyeka,
Ila hili la faradhi, kulikosa nateseka,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Si elimu sio kazi,sioni kinachofanyika,
Maisha sasa upuuzi,natamani kuondoka,
Ningelipata jahazi,nami ningejumuika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Hayanitoshi makazi,hapana panapokalika,
Lanijia jinamizi,usiku ninateseka,
Nachelea kuwa chizi,usiposhughulika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Yanalowana malazi, kitanda kinafurika,
Na mto huu siuwezi,umekwishasambaratika,
Na godoro hili uzuzi,ja kikojozi katwika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Wanaofutwa machozi,walahi wafarajika,
Hawanacho kizuizi,kupendwa watapendeka,
Ila mie sinakazi, ila ni kulalamika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Hadithi siimalizi, kwiki imeshanishika,
Jamani tena siwezi, sijui wapi pa kushika,
Natamani kwenye ardhi, sasa ningelimezeka,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Yamenifika mtunzi, kumtaka asokutaka,
Nimejikuta bazazi, watoto wananicheka,
Mgonjwa sina muuguzi, nazidi kusononeka,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

No comments: