Tuesday, September 14, 2010

Leo waula Mseto

Walishasema hawali, hawautaki mseto,
Tukakiomba kibali,cha wale wenye uoto,
Diwani na maliwali,wakafanya mchakato,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Walidhani mweupe wali, ndio mapishi ya moto,
Hawakujua rijali, pilau wala mseto,
Na wapishi wenye akili, wakautangaza wito,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Wakaiteta shughuli, na kuubeba uzito,
Mioyo wakaibadili, na ndimi zenye mnato,
Hapakuwa na bahili, kwa wazee na watoto,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Azimio bilkuli, likapata manukato,
Waume na wanawali, wakakataa masuto,
Haramu siyo halali, imani yetu si ndoto,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Waliosema hawali, leo waula mseto,
Tena wameukubali, wapiga kubwa makato,
Nisai na marijali, hawanao mchecheto,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Mpinzani sasa chali, keshalikosa vukuto,
Wadau wake hawali, njaa yawapa majuto,
Walaji yao kauli, wapishi wana mvuto,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Baada ya maankuli, utakuja mchanyato,
Miseto kuibadili, tofauti mitokoto,
Ili iwe kulhali, yaleta kubwa mvuto,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Wasijione dhalili, wala kuwa ni watoto,
Akheri yataka akili, na sio ndoto za mto,
Hufaulu ikibali, wenye kusaka ukweli,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

Hapa nateta kamili, nimeshangilia wito,
Yamebakia maswali, kufanzia mkokoto,
Subira ipe sabili, jibu laitwa mseto,
Leo waula mseto, na walisema hawali.

No comments: