Tuesday, September 14, 2010

Upendwapo

Ukipendwa nyenyekea, nawe utazawadiwa,
Kiburi ukijitia, pendo utalibomoa,
Ukishikwa shikilia, na sio kujiachia,
Upendwapo badilika, au utasahaulika.

Apendwaye hulegea,wala si kukakamaa,
Ukiitwa itikia, si swali kuulizia,
Ukidakwa ng'ang'ania, au utabdanduliwa,
Upendwapo badilika, au utasahaulika.

Ukipendwa shikilia, ina uchoyo dunia,
Hili ukiliachia, mengine yanapotea,
Ukiimeza hadaa, utatapika knyaa,
Upendwapo badilika, au utasahaulika.

Ukipendwa chekelea, si mashavu kupembua,
Tabasamu yako njia, hata mzigo ikiwa,
Ichunge yako hatua,mijoka inatambaa,
Upendwapo badilika, au utasahaulika..

Ukipendwa mwana kuwa, si utoto kubakia,
Akili kuzinyanyua, majukumu kuyajua,
Chini ukishabakia, zaidi hudidimia,
Upendwapo badilika, au utasahaulika..

Ukipendwa ng'ang'amua, vitendawili agua,
Uzito ukizidia, huliangusha gunia,
Na mguu hutoinua, mbele kuja endelea,
Upendwapo badilika, au utasahaulika..

Ukipendwa changamkia, tenda haitachelewa,
Jifunze usilojua, na ujinga kuukimbia,
Huna pa kuegemea, ila mbora ukawa,
Upendwapo badilika, au utasahaulika..

Ukipendwa tumikia, kila unalogharamiwa,
Na fikra kupakua, unyumba kujijengea,
Gundi na nta kutiya, kuta zikatengemaa,
Upendwapo badilika, au utasahaulika.

No comments: