Thursday, September 16, 2010

Ndio ukubwa wa pua

1.
Laiti ingelikuwa, pua kubwa damisi,
Watoto wasingekuwa, wanatoka makamasi,
Udogo ungezidia, katu wasitanafusi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
2.
Humkuta babu pua,michirizi yamuasi,
Kila akilipengua,maji yanamdadisi,
Huugua akalia,sikuzote wasiwasi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
3.
Pua ndogo hutulia,na mabonge kuanisi,
Mtoko hukushtua,kama skadi ya Mrussi,
Na ubongo hupagawa, kwa raha unavyohisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
4.
Kama hili watambua,mja umeshadurusi,
Dunia kweli wajua,ma ukweli wake kiasi,
Kiumbe hajatimia,bila hii fahirisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
5.
Upepo ukipepea,kifua mara huasi,
Na nusura ni mafua,mirija yake kamasi,
Uchafu huuchukua,kuupitisha kwa kasi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
6.
Kamasi ukilitoa,huburudika nafsi,
Kitu kidogo twajua,lakini yote Qudusi,
Rehema zake zatua,japo tuna Ibilisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
7.
Pua yangu nilidhania, imeshapita kiasi,
Ukubwa imezidia, itajakuwa nuksi,
Wazungu nikashangaa, zao kwao kama basi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
8.
Ndipo nikang'amua,pua kubwa si mkosi,
Ukitaka kuendelea,uwe yake majilisi,
Mashine utavumbua,na madawa kuasisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
9.
Pua iliyodumaa,zinaleta uyabisi,
Hawana wanachojua,akili zao muflisi,
Ni watu wa kununua,kutengeneza hadithi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
10.
Hata waitwao mapua,hili kwao si nemsi,
Ovyo wameshakuwa,fikra zao najisi,
Kila wakijifaragua,wawashinda ubinafsi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
11.
Kila nikifikiria, baridi ninaihisi,
Mwafrika sijamjua, kuitaliki nafusi,
Lake ndilo maridhia, ya wengine si mfuasi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
12.
Msaada tungegawiwa, tena ulo mahsusi,
Pua tungezawadiwa, tupunguze ubinafsi,
Na wengine kuangalia, maisha yawe harusi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
13.
Ni kazi kuendelea, budi utoe kamasi,
Sie tunadidimia,pua zimekosa jasi,
Uongo tunapumua,na mipango ya nuksi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
14.
Lipi tumeshikilia,si sanaa si sayansi ?
Ni watu wa kusaidiwa,kwa viatu na libasi,
Watu wa kuhurumiwa,kwa haramu na najisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.

No comments: