Wednesday, September 15, 2010

Tofauti ya mjanja

Trekta moja latosha, mjanja kutengeza mengi,
Gari moja humuwezesha, kuleta yake shangingi,
Kompyuta mbili tosha, kuziunda zake nyingi,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Simu chache zinatosha, kuunda chake kiwanda,
Mtambo uliokwisha, wa mgodi huko Rwanda,
Mjanja humuwezesha, mitambo yake kuunda,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja huona nje, hatafuni tu vya ndani,
Ili watu asipunje, ajua kwenda ugenini,
Yeye sio mwana njenje,ufukara sio chanda,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hampi kazi, mgeni mwenyeji afe,
Hana jana wala juzi,halisimami lake tufe,
Na mjomba na shangazi,kwa hili moyo wasife,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja si mnunuzi, bali mtengenezaji,
Kama sivyo mchuuzi,huu ndio wake mtaji,
Kuelea ndio hadhi,mjinga aenda na maji,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja mali yake watu, mjinga maliye vitu,
Pakizuka utukutu, hujikuta ni kiatu,
Mwenye mbili si tatu,na jembe haliwi ratu,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja huishi pacha, kama hai kama mfu,
Nalo kwake si Alinacha,bali wingi wa sharafu,
Mcha Mungu hatoacha,hali hii kuiafu,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hayahujumu, kamwe yake mazingira,
Na kwalo akikutuhumu,kali yake hasira,
Huwa wakati mgumu, kwako kupata maughufira,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hawaajiri, fala na wasiojua,
Huwa hachezi kamari, na mradi wenye ulua,
Malengo yake kadiri,ujinga hakuzoea,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hawi kipofu, mkataba akisaini,
Kwake hili la wakfu,hakubali uzaini,
Hucheza yake turufu,nchi yake huthamini,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja sio fisadi, wananchi kuwaibia,
Wala sio mkaidi, nchi kuwaharibia,
wala sio mritadi, ukoloni kurudia,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hawi mfumo, kila kitu kutawala,
Ajua chake kikomo, desturi pia mila,
Na huzuni na nderemo, kwake hayana kabila,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Kila mtu ana zake, wahenga wasema nywele,
Waume na wanawake, wazima na wenye ndwele,
Mwanzo, mwisho ni mwnenzake, na chini ina kilele,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

No comments: