Wednesday, September 15, 2010

Mipango mji

Mji mipango wataka, kila hali kuvutia,
Si nyumba tu kujengeka, bali pia na majaa,
Misingi bugi kuweka, iwe misafi mitaa,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Kazi kustaarabika, ni vita kupigania,
Hujui wanakotoka, watu wanaoingia,
Tofauti ya hulka, pia nayo mazoea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Sheria budi kuweka, watu kuwasimamia,
Yawe yanayofanyika, kote yanakubaliwa,
Na yasiyokubalika, watenzi kuadhibiwa,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Haiwezi kujengeka, miji isiyotulia,
Mabomu yatalipuka, watu wabaki walia,
Uchafu utatukuka, uozo ukaenea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Na maji yatamwagika, hakuna wa kuyazoa,
Mioto italipuka, maafa yakaingia,
Magonjwa yatalipuka, watu wengi kupotea
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Mwenyeji hufurahika, mji msafi ukiwa,
Huacha kulalamika, sifa nyingi kuzitoa,
Watoto hushereheka, mji wao kujivunia,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Wageni humiminika, kuja kuwasalimia,
Miezi hadi miaka, wakawa wanaoingia,
Mji hugeuka Makka, Hija watu kuhijia,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Watalii watafika, na sifa nyingi kutoa,
Wengine huwaalika, kuja kututembelea,
Kipato kikaongezeka, shida zetu kupungua,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Diwani mnuka taka, hafai kuvumilia,
Mtaa huaibika, naye kadhalika pia,
Mtupe kwenye kichaka, kisha na moto kutia,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Meya kama takataka, nini awasaidia ?
Harufu mbaya huweka, na nyie mwapendezewa?
Uoza mkiutaka, magonjwa huwatembelea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Mbunge mwenye kunuka, huleta harufu mbaya,
Jimbo halitokalika, ushuzi unaonukia,
Vipi huyu mwamuweka, au nyie zimepungua?
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Wakuu wanahusika, wa mikoa na wilaya,
Kukosa kustaarabika, nao wanavumilia,
Hawa watu wa mashaka, mbele hatutasogea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

No comments: