Thursday, August 19, 2010

Kusali si ucha Mungu

1.
Sali na kutumikiya, sala sio ubinafsi,
Sali ukiwajulia, sala sio muflisi,
Sali ukisalimia, sala sio ujasusi,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
2.
Sali saa ishirini, utazipata thawabu,
Za sala kama makini, hilo halina taabu,
Binadamu ukihini, zinapungua thawabu,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
3.
Kusali hii faradhi, nani asiyeijua,
Ila walio na maradhi, wataka kuhudumiwa,
Na wewe ukiwa radhi, ucha Mungu watimia,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
4.
Kusali jambo la heri, shetani akukimbia,
Ila kama wewe tajiri, masikini saidia,
Na hata kama fakiri,wape wakikujia,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
5.
Kusali ibada njema, mayatima bora zaidi,
Ukiwafanyia dhuluma,ibada huifaidi,
Hukusubiri kiama,ya madai na ukaidi,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
6.
Ukiwanyima wajane, haki wanazostahili,
Sali ishirini na nne, sala zilizo kamili,
Hakika ni kama mavune, mtihani unshafeli,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
7. .
Wazazi ukiwaasi, au kutowasaidia,
Tena na wewe mkwasi, shida hujaijua,
Sali bila wasiwasi, kitu hutoambulia,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!
8.
Fisadi uliyetimia, na sigda kubwa nyeusi,
Maghufira kukuombea, lazima tunajihisi,
La sivyo umeangamia,Adilizo zina nakisi,
Kusali si ucha Mungu, ucha Mungu ni vitendo!

No comments: