Thursday, August 19, 2010

Tikitaka

1.
Kafunga kwa tiktaka, kipa kachanganyikiwa,
Hajui lililomfika, adui ashangilia,
Nyuma akijageuka, beki mpria azoa,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
2.
Kipa hakuwa na shaka, goli halitaingia,
Lakini yamemfika, asiyoyatazamia,
Kiuno bado kashika, dunia kaichukia,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
3.
Ni goli la tiktaka, mshambulizi kaambua,
Za majeruhi dakika,ndizo zilizosalia,
Kipengo kitapigika,sekunde zikitimia,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
4.
Wachezaji waweweseka, kati hawajasogea,
Refa mwenyewe kaweka, katikati kuanzia,
Na sasa anasumbuka, wajipange kwa hatua,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
5.
Kocha tama ameshika, tumaini lapotea,
Kibarua akitaka,majani chamuotea,
Miujiza anataka,kiwanjani kutoke6a,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
6.
Filimbi imealika, mpira umezubaa,
Mwishowe wanagutuka, unaanza kutambaa,
Popote haujafika, filimbi inakataa,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
7.
Hoi hoi wanacheka, wapinzani wafurahia,
Bingwa keshafungika,tiktaka kutojua,
Mambo mchakachaka, nderemo za kushangilia,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
8.
Mmachinga tiktaka, golikipa manispaa,
Gwiji anafungika,na ushindi aotea,
Hana lililo hakika, la kufanya hajajua,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
9.
Kutenda bila fanaka, mzigo wenye balaa,
Kusoma bila kushika, huna utakalolijua,
Kufanya bila hakika, huwezi kufanikiwa,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
10.
Wenzako wanalolitaka, wewe ukalikataa,
Hukuona ni dhihaka, mbwa koko wa karaha,
Na kazi yake kubweka, mwizi humkimbia,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
11.
Uongozi wa mashaka, matatizo huyazua,
Sio wa kuaminika, matatizo kutatua,
Badala yake huruka, maji kinyesi kuvaa,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!
12.
Tafakari madaraka, si watu kunyanyapaa,
Watakiwa kuwashika, uwafae watakufaa,
Watakiwa kuwadaka, na goli halitaingia,
Ni goli la tiktaka, golikipa hajajua!

No comments: