Thursday, August 19, 2010

Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.

1.
Utu si ubinadamu, mshairi ninasema,
Utu ni jambo adimu, wengi wameshauhama,
Viumbe ni binadamu, lakini utu lawama,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
2.
Utu si ubinadamu,itazameni kalima,
Utu ni kitu adhimu, Mola wengi kawanyima,
Utu wataka Halimu, na kubwa ndani hekima,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
3.
Utu ya juu nidhamu, utadhani ni karama,
Utu ya haki hukumu,bila kugwaya uhasama,
Utu adili nadhimu, uadiifu wa dawama,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
4.
Utu ni kutakadamu, mwenendo na tabia njema,
Utu ni uislamu, fundisho mpaka kiyama,
Sio wote wanadamu, utu wapewa heshima,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
5.
Wapo vinara hakimu, viongozi wa heshima,
Kadhalika wanajimu, nyota waliozisoma,
Ila utu madhulumu, hawana cha chini kima,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
6.
Wapo mashehe na walimu, na mapadri waadhama,
Jichoni ni binadamu, kubwa twawapa heshima,
ila nakisi yadumu, utu kwao umehama,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
7.
Twawaona binadamu, utu vipofu nasema,
Utu sio la ghanimu, wala kwa cheo kuvuma,
Maskini huwa rahimu, malaika kumpema,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.
8.
Mtoto huufahamu, mkubwa kutokuusoma,
Mjinga huwa karimu, mwenye akili kuzama,
Nisai huwa hirimu, rijali akachutama,
Utu si ubinadamu, wasomi watupoteza.

No comments: