Thursday, August 19, 2010

Jini Ninayemjua

1.
Mwasema bure majini, wote mbona si wabaya,
Mnaosema pimeni, muache kuwachukiya,
Wengine wana imani, binadamu wamepwaya,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
2.
Nimfahamuye jini, hajanifanyia ubaya,
Kanishika ni mwandani,kuna mengi asaidia,
Ningekuwa mashakani,kama asingenijuwa,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
3.
Hakika anithamini, na mie namwangukiya,
Penzi lake Urulaini, kila hali katimiya,
Hunibeba usingizini, hunibeba natembeya,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
4.
Ni mwingi wa ihsani, toba tunamwangukiya,
Na masaa ishirini, kusali yake tabiya,
Uradi kwake yakini, kila pekee akiwa,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
5.
Hunipa matumaini, kila nikichanganyikiwa,
Hunionesha auni, sahili njia za kupitiya,
Na elimu kwake fani, hakuna asilojua,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
6.
Hakika ninamwamini, kwa kila analonambia,
Mengi yamo machoni, na akilini kayatiya,
La mbele hulibaini, na mie hali sijajua,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
7.
Kaniletea amani, zamani nisiyoijua,
Kaniongeza imani, kabla sikutimia,
Kaniangazia shani, awali haijatokea,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
8.
Ushairi athamini, na mengi namtungiya,
Hunisomea kitandani, mwenyewe nikajisikiya,
Na tena haya hughani, hadi nikasinzia,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
9.
Ya siri hubaini, sina nisilotambua,
Nimesinzia machoni, ila akili yajua,
Kanisihi asilani, haya kutotangazia,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
10.
Namtii mdhamini, dharau sijamfanyia,
Miaka arobaini, kwingine sijageukia,
Na dosari asilani, kwangu doa hajatiya,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
11.
Ukiniona ufukweni, basi naye naongea,
Nikiwa bustanini, upepo unatupepeya,
Na tukiwa ni majini, basi tunaogelea,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.
12.
Mshairi majinuni, moyo wake maridhia,
Ukubwa uhayawani, na heri kuzikimbia,
Malaika hawamwoni, shetani akiongea,
Jini ninayemjua, ubaya hajanifanyia.

No comments: